JE, UKAWA UTASHINDA KAMA APC NIGERIA?
Umoja Wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA) ni umoja ulioanzishwa na baadhi ya vyama pinzani nchini
Tanzania vikiwemo CHADEMA, NCCR, CUF na vingine.
Umoja huo unafanana na
umoja ulioundwa na vyama vikuu vitatu vya upinzani nchini Nigeria ambavyo
viliungana mnamo mwaka 2013 ambavyo ni Action Congress of Nigeria (ACN), the
Congress for Progressive Change (CPC), the All Nigeria Peoples Party (ANPP)
,All Progressives Grand Alliance (APGA) na kuunda umoja unaoitwa All
Progressive Congress (APC) ambao ulimpa ushindi Rais Muhammadu Buhari dhidi ya aliyekuwa
rais Goodluck Jonathan.
Lengo la umoja huo ni
kuunganisha nguvu za wanachama wa vyama hivyo ambao watakuwa na nguvu moja hata
katika kupiga kura utakapofika uchaguzi mkuu mwezi September mwaka huu.
LOWASA
KUJIUNGA UKAWA
Wachambuzi wa mambo
wanasema umoja huo umeongeza nguvu zaidi hasa baada ya hapo jana tarehe 28
Agosti mmoja kati ya kada mkubwa wa CCM na aliyewahi kuwa waziri mkuu Edward
Lowasa kujiunga na CHADEMA ambacho kipo chini ya mwavuli wa UKAWA.
Kujiunga kwa Lowasa
kunatajwa kuwa huenda yakawa mafanikio makubwa kwa kuwa ana wafuasi ambao
watalazimika kumfuata na kuunga mkono juhudi za UKAWA kukiangusha chama tawala.
Kuhama huko kwa Edward
Lowasa kunatajwa kuwa ni kutokana na jina lake kukatwa katika listi ya watia nia
kupitia Chama Cha Mapinduzi jambo ambalo kwa upande wake aliliona kama ni kukatiza
ndoto zake za kuwa Rais.
Muungano wa UKAWA
unafanana na Muungano wa nchini Nigeria uliowafanya wapiga kura wa vyama hivyo
tofauti vilivyoungana kumpigia kura mgombea mmoja aliyesimamishwa kugombea na
hiki ndicho wanachokilenga UKAWA kwa kuangalia mtu anayekubalika katika eneo
husika na kumsimamisha kuwa mgombea.
Umoja huo unaongeza
nguvu kwa vyama pinzani kwa maana ya kwamba mgombea atakayeteuliwa na umoja huo
atapigiwa kura na wanachama wa vyama vyote vinavyounda umoja huo.
Tumeshuhudia katika
uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi wa 12 mwaka 2014 upinzani ulipata viti
vingi kuliko miaka ya nyuma hivyo hii inaweza kutafsiriwa kuwa Muungano wao kwa
jina la UKAWA ulifanikisha kuongeza nafasi ya ushindi.
UKAWA ulianzishwa mnamo
mwaka 2014 wakati wa mchakato wa kuchambua na kupitia rasimu ya katiba
iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa tume ya Rasmu ya katiba iliyopewa jukumu ukusanyaji
wa maoni juu ya katiba mpya Jaji Sinde
Joseph Warioba.
Kutofautiana itikadi na
mawazo kati ya wawakilishi waliochaguliwa kujadili rasimu hiyo ambao wengi wao
ni wabunge na watu kutoka taasisi mbalimbali kulipelekea baadhi ya wawakilishi na wabunge kutoka vyama pinzani
kususia mchakato huo na kudai kuwa umechakachuliwa kwa kuondoa baadhi ya maoni
ya wananchi.
Tukirudi Nigeria Umoja
wa APC ndio ulimpa ushindi Muhammadu Buhari na kuwa Rais wa Nigeria baada ya
kumuangusha Rais Goodluck Jonathan wa chama tawala cha PDP hivyo swali lililopo
ni je, nguvu ya UKAWA itaweza kukiondoa
Chama Cha Mapinduzi?
By Benezeth Kahwa
0766522469

No comments